VIJIMAMBOZ PROUD AFRICAN KASRI LA MWANAZUO BONGOCELEBRITY NKYA MAWAZO NA MAWAIDHA JIKOMBOE MIRUKO NDABULI SHAMIM ZEZE DAMIJA MATERU MLOYI CHEMI CHE MPONDA BAKANJA MTAFITI LUKWARO MSANGI MDOGO MARK MSAKI DIRA YANGU MWAIPOPO KONA YANGU FURAHIA MAISHA YAKO DAMIJA MICHUZI FATHER KIDEVU MWANDANI NGURUMO FATMA KARAMA ZAINAB OMEGA NGOLE YAHYA CHARAHANI JARIDA LA UGHAIBUNI NYEMBO BWAYA BHALEZEE JUNGU KUU WATOTO WETU BLG BROTHER SAA YA UKOMBOZI NURU AKILINI TAFAKARI ZA MAISHA ALBERT WILSON UCHUMI MIDRAJI IBRAHIM Lucassano CHESI HAKI NGOWI KISIWA CHA AMANI Innocent Kahwa SULTAN TAMBA SIMON KITURURU MAVIZO MUSA NGARANGO KIJIWENI(NED) WATANZANIA JADOUNG METTY MAGGID MJENGWA SAHARAN VIBE MWENYE MACHO ABDALLAH MRISHO MYAFRICA SHERIA NA MAVAZI
NEW VISION UGANDA MONITOR UGANDA KENYAN NATION MEDIA EASTANDARD FROM AFRICA BUSINESS WEEK ALL AFRICA
MAGAZETI YA IPP UHURU NA MZALENDO BUSINESS TIMES DAILY NEWS TANZANIA DAIMA MWANANCHI BUNGE LA TANZANIA SERIKALI YA TANZANIA IPS INTERNATIONAL
AFRIKA HURU NINI KILITOKEA PAMBAZUKA DUNIA YETU GADO CARTOONS
SEND ME AN E-MAIL
Friday, February 06, 2009
UNA WAZO ZURI?WAAMBIE WENZAKO!

Kila siku mimi hupenda kupitia tovuti mbalimbali.Huwa napitia takribani tovuti mia mbili kila siku.Lakini ninavyozipitia mimi ni kwa kutumia huduma ya bloglines.Kama tovuti ina kitu kipya basi jamaa wa bloglines hunishtua ili niicheki.Kama hakuna kipya basi naachana nayo kwa siku hiyo au saa hilo.

Ninapopitia tovuti mbalimbali huwa napata mawazo,mengine mazuri na mengine mabaya.Bahati nzuri ni kwamba chaguo huwa siku zote linabakia kwangu.Zile zenye mawazo mabaya kama vile ya kibaguzi nk huwa nachagua kuachana nazo.

Lakini pia huwa napitia tovuti zenye mawazo mazuri sana.Wakati mwingine huwa natamani nimwambie kila mtu kuhusu wazo zuri nililolisoma au lililonijia baada ya kusoma au kuona kitu fulani iwe ni mtaani au kwenye luninga.Labda ndio maana napenda misheni za habari na mawasiliano.Kimsingi ni kubadilishana mawazo.

Mnamo mwaka 2000,jamaa mmoja anayeitwa David Owen alianzisha mtandao unaokuwezesha wewe,mimi na yule kuweka mtandaoni mawazo yoyote mazuri ambayo tunayo,tumekuwa nayo siku zote au ambayo ndio kwanza tumeyagundua baada ya maongezi na babu na bibi pale kijijini ulipowatembelea.Tovuti yake aliita idea-a-day.Unaweza kuitembelea kwa kubonyeza hapa.Ukishafanya hivyo jiunge ili uweze kupata wazo au mawazo mapya kila siku kutoka kwa watu wengine duniani.Kumbuka kila kitu kilichowahi kufanywa au kinachotarajiwa kufanywa siku za mbeleni kilianzia kwenye "wazo".
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 8:06 PM | Permalink | Maoni 23
Wednesday, December 31, 2008
KHERI YA MWAKA MPYA

Ingawa hatujaonana hapa kijiweni kwa muda kiasi,natumaini kwamba hujambo na Mungu amekujalia kuuona mwaka huu wa 2009 ukiwa mwenye siha njema kabisa.Nikutake radhi kwa kunikosa kwa muda mrefu.Mipangilio ya kiutendaji,majukumu,afya,familia na mambo kama hayo ndio chanzo cha kimya changu.

Kwa sababu huu ni mwaka mpya,basi bila shaka nitajitahidi kutimiza lengo hili la kuandika hapa mara kwa mara kadri nitakavyoweza.Ingawa naendesha blog zingine,blog hii ya harakati inabakia kuwa lulu kwangu.Hapa ndipo nilipoanzia safari yangu ya ku-blog.Hapa ndipo cheche(kama zipo) za mawazo na mtizamo wangu kijamii zilipoanza kuonekana rasmi.Siwezi kupakacha kamwe.

Mwaka mpya huwa ni wakati wa malengo mapya na mwelekeo mpya.Kila binadamu ana malengo yake hapa duniani.Mimi nina malengo yangu na wewe pia una yako.Kila kukicha huwa tunajitahidi kuyatimiza.Tunapasua vichwa kujaribu kuyatimiza malengo yetu.Ndio maisha.

Bila shaka na wewe umeshaketi chini na kujiuliza swali hili;ninataka kutimiza malengo gani mwaka huu?Je ni kurudi shule kuongeza ujuzi?Je ni kuoa au kuolewa?Je ni kujitolea zaidi katika jamii yako?Je ni kutunza na kulinda mazingira?Msururu wa malengo unaweza kuwa mkubwa.Kama kutimiza malengo fulani fulani ndio mkakati wako wa mwaka huu basi zingatia ushauri ufuatao;
  • Weka malengo yanayotimizika au yenye uhalisia-Jiangalie ulipo,angalia vitendea kazi ulivyonavyo,tizama kwa makini ujuzi ulionao kisha yapime vizuri malengo yako.
  • Jiulize swali au maswali;Nitayatimizaje malengo yangu?Ukishafanya hivyo jiwekee utaratibu wa jinsi ya kutimiza malengo yako.Wazungu wanasema weka vyema Action Plan yako.
  • Nenda taratibu-Mwaka ndio kwanza umeanza,yakaribie malengo yako kwa mwendo wa taratibu.Usiwe na haraka wala pupa.Si unakumbuka kwamba mambo mazuri hayataki haraka?
  • Usiogope kurekebisha malengo-Kadri mwaka unavyoanza kusonga mbele,unaweza kugundua kwamba huenda usiweze kutimiza malengo fulani.Hiyo inawezekana kutokea kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi,kiafya au kibinafsi.Usihofu kurekebisha malengo yako.
  • Usiogope kushindwa-Yawezekana kabisa ukashindwa kutimiza malengo fulani fulani.Sababu zaweza kuwa kama hizo nilizozitaja hapo juu.Usiogope.Cha muhimu ni kujaribu na kujaribu na kujaribu.Jitahidi kadri unavyoweza.Nina uhakika ukijaribu utafanikiwa kwa hiyo mwisho wa siku hadithi ya kushindwa wala haitokuwepo.
  • Omba msaada inapobidi-Yapo mambo mengine ambayo hutoweza kuyatekeleza peke yako.Hilo linapotokea,usiwe mgumu kuomba msaada.
Kwa msaada zaidi unaweza kutumia tovuti kama ya mygoals.com.Nakutakia kila la kheri katika mwaka huu wa 2009.Tutaendelea kukumbushana.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 8:35 PM | Permalink | Maoni 7
Sunday, April 27, 2008
MALCOLM X: BALLOT OR BULLET
Umeshawahi kumsikia...au japo kulisikia jina lake. Dunia ilikuja kumtambua kama Malcolm X. Sasa kama umeshawahi kuwa na kiu ya kumtambua vyema au kujua alichokisimamia, sikiliza hotuba yake hiyo hapo chini aliyooita Ballot or Bullet.Kisha baada ya kusikiliza,jiulize; alichokiongelea kina uhusiano wowote na maisha tuliyonayo hivi leo?

 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 9:54 AM | Permalink | Maoni 6
Friday, February 08, 2008
HII NDIO BONGO BWANA!

Leo siwezi tena kuomba msamaha kwa kutokuandika hapa mara kwa mara.Kama mnataka na mimi nijiuzulu kama waheshimiwa huko Tanzania….we acha tu.Vyeo vitamu bwana…si mlisikia wenyewe jinsi sauti za waheshimiwa zilivyokuwa zikitetemeka na kujaa mwangwi wakati wakitangaza kujiuzulu? Si mliona pia jinsi wengine hadi wake zao walivyoangua chozi?Unafanya mchezo nini? Hapo mimi ndipo ninaposhangaa,kama cheo au ukubwa unaupenda hivyo,kwanini usiwe mwadilifu basi?Eti kwanini? Kama wewe unajua kwamba hapa duniani unapenda kubebewa briefcase,unapenda kufunguliwa mlango wa gari na wa nyumba,unapenda kufungwa mkanda kama vile mtu uliye hoi kitandani,kwanini unaleta uzushi na uzabinabina unapokuwa madarakani?

Okei,sasa jamaa wametangaza kujiuzulu,mkuu wa nchi kakubali maombi yao..what next? Next ni kwamba jamaa bado wapo bungeni,tena bado wanachangia mijadala.Hii ndio bongo bwana.Changa la macho kama kazi. Hivi si ni ajabu kwamba unapojiuzulu,baada ya kukumbwa na kashfa nzito kama ya ufisadi,ubunge nao unatakiwa ukome mara moja? Mpiga kura gani anataka kuendelea kuwakilishwa na “fisadi’. Halafu Tanzania hamna hata ile sheria ya kuweza kum-recall mbunge.Yaani mkishamchagua,mnalo kwa miaka mitano.Linakuwa tsunami lenu tena. Halafu huko bungeni aliyemwaga manyanga jana leo anachangia na kusema Rais amechagua “mtu kama mimi”.Yaani wazi wazi kabisa mtu anasema,mmeuvaa tena mkenge.Na anapigiwa makofi na virungu! Ee bwana ndio…hii ndio bongo…kila mtu inabidi ajifanye hamnazo ili angalau kesho aweze kuamka na kwenda kazini. Hebu kwanza cheki hapo kama umeme upo bado au ushakata na kompyuta yako inatumia ule wa kudandia tu unaposoma habari hii.

Haya sasa,PM mwingine huyooo..anajinadi..anasema yeye ni mtoto wa kwanza(hata sijui hii inahusiana na nini).Anasema yeye ni mtoto wa mkulima.Alikuwa au bado ni mtoto wa mkulima? Kiswahili lazima tukitanue wajameni.Ahaaa…kumbe huyu naye anatoka pale pale…yaaani pale pale kwenye ofisi ya waziri mkuu! Halafu sura ni miongoni mwa zile zile.Bila woga na yeye anasema kumbe keshakaa sana pale ikulu..yaani anapajua kuliko hata nani sijui. Sasa hapo ndipo utakapochoka…kumbe sasa nini kipya hapa? Hapo hujazingatia jinsi mambo yalivyokwenda fasta? Hivi unataka kuniambia mambo yote haya,kimstakabali wa nchi..nasema nchi sio kijiji,yanafanyika ndani ya masaa kama 16 tu?? Kama ni kweli basi nchi yetu inastahili medani ya hali ya juu sana kwenye suala zima la disasters preparedness.

Wale wanaoitwa wapinzani…masikini hawa nao naona wamepigwa ganzi kiaina.Yaaani hata kuguna hawakuguna! Ingekuwa mimi ningesema haya ninayoyasema hapa.Eti nini…anaitwa nani?Pinda? Ofisi ya nani..Waziri Mkuu?

Sasa subiri baraza jipya la mawa-siri.Hapo ndipo utaweza kuthibitisha hizi hoja zangu.Kama unabisha tizama kama yule jamaa mwenye jina linalohusiana na vita vya majimaji hatarudi tena kwenye “kebineti”.Ni kama vile hakuna watu wengine wanaoweza kuwa mawaziri na manaibu waziri.Utasikia tu.Tena nasikia ule msururu wa mawaziri unarudi tena,tena na zaidi.Hii ndio bongo.

Aisee ukiona kimya sana hapa usidhani nimetoweka duniani..huwa pia naandika pale http://bongocelebrity.com.

 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 7:39 PM | Permalink | Maoni 8
Friday, January 11, 2008
JINSI YA KUIBA UCHAGUZI/KURA

Hadithi za chaguzi zisizo huru barani Afrika zinazidi kuwa kama vile hadithi za kila jioni alizokuwa akitusimulia bibi wakati wa utotoni. Si unakumbuka zile;jioni baada ya msosi bibi anawaweka pembeni ya moto na kutupigia hadithi tamu.Wakati mwingine tulikuwa tukisinzia kutokana na uchovu na wakati mwingine hatukuthubutu hata kupekua kope kwa jinsi hadithi zilivyonoga.Binafsi nilikuwa natoa macho zaidi kama hadithi inakuwa ya kutisha tisha hivi.Uoga!

Tofauti ni kwamba hadithi za bibi zilikuwa na mafunzo tele.Kila jioni tulipenda kuzisikia kwani zilitupa maarifa na elimu ambayo Mwalimu yeyote yule shuleni asingeweza kutupa.Kwanza walimu walikuwa wanapenda sana mchezo wa kuchapana.Ukikosea kidogo tu,unacharazwa viboko.Nadhani walikuwa wanatumia staili ya kimarekani-kutishana,kupigana mkwala ili kuzibana mdomo na kuendelea kutawala.Lakini si unakumbuka jinsi na wewe ulivyokuwa mjanja kwa “kujaladia”? Hujaelewa? Namaanisha kuvaa nguo kadhaa ndani ili viboko vifanye kudunda tu…Okay nasema hadithi za bibi zilikuwa hazichoshi.Hizi habari za chaguzi zisizo huru zinachosha. Kama hujachoka kuzisikia ni wazi umekuwa ukiangalia zaidi sinema badala ya taarifa za habari.

Kinachotokea nchini Kenya hivi sasa ni mwendelezo tu wa wizi wa kura na demokrasia.Ndio maana jamaa mmoja amesema labda demokrasia sio mambo ya kwetu.Hatutaki au hatutakiwi kuwa na demokrasia. Huyu tumemjia juu,tumemuuliza mbona hata huko kwa bwana mkubwa (US) raisi wao hakuchaguliwa na wananchi bali mahakama? Sasa nani wa kumvalisha paka kengele?Mwai au Kichaka?Hapo ndipo mchezo unapokuwa mgumu.Si ndio maana mumewe Lucy kakataa hata kufuata ushauri wa yule mwakilishi? Mwakilishi alipofika na kushupaza mishipa kwa mumewe Lucy,jamaa akacheka sana.Akamwambia look who is talking.Likawashuka!

Sasa ni jinsi gani mtu anaiba uchaguzi?Kama ulifuatilia kilichojiri Kenya, ni wazi utakuwa umepata picha mbaya kuliko.Hata negative huwa haipo hivyo.Kilichofanyika pale ni uhuni,wa wazi wazi kabisa.Halafu jamaa wakasimamisha ndude zao wakasema “mwanaume kweli apite mbele”.Jamaa wanavyoogopa habari za “popo bawa” wote wakanywea.Ngoma bado mbichi.Kitakachotokea jumatano ijayo tunasubiri kuona. Lakini nahisi hata kule kwa bwana Madevu aliyeuawa bila kwa hatia hiyo hiyo ya wahukumu na wanyongaji wake kutakuwa salama.

Hata twende sasa. Ukitaka kuiba uchaguzi au kura kwanza unachotakiwa kufanya ni kuchagua mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ambaye ni swahiba wako.Kisha unampa maelekezo kwamba makamisaa wote wawe ni watu mnaojuana.

Pili wale ambao unadhani watapigia kura wapinzani wako unawaundia kesi.Kesi za kutunga zipo kibao.Msingizie kwamba kachukua rushwa au kabaka vitoto vidogo.Yeye na wanae wote.

Tatu kwenye daftari la wapiga kura weka majina unayoyajua wewe.Waliokufa,walio chini ya umri wa kupiga kura nk…wote twende kazini.

Jamaa wa nje wakisema wanaleta wasimamizi wa kimataifa waambie kumeshajaa.Hakuna nafasi.Waambie tayari unao wasimamizi wa kutosha.Wakikuuliza wanatoka wapi usiwafiche.Waambie ukweli kwamba wasimamizi wako wanatoka China,Urusi,Iran,Zimbabwe nk.

Kisha tumia watu kama wanajeshi na wanausalama.Wote hawa siku hiyo wapigishe kura hata kama sheria inasema vinginevyo.Si unajua kule ni amri kwanza maswali baadaye?Eenh fanya kweli hapo.

Usisahau kuongeza “vituo vya kupigia kura” viwe maradufu.Weka vituo mpaka kule ambako una uhakika hakuna mgeni yeyote anaweza kuthubutu kufika.Kule Ngalilo ndani ndani huko.Sema kuna wananchi kibao huko wamekuchagua kwani wanasema umewapelekea maendeleo mengi sana.Umepeleka vyandarua huko kwa sana tu.

Kama vyote hivi vinashindikana basi fanya kama mumewe Lucy.Mwambie mshikaji wako atangaze kwamba umeshinda.Kisha,bila kuchelewa, jiapishe.Usisubiri upuuzi wa kualikana kwa ajili ya sherehe za kuapishwa zilizo na gwaride na hotuba ndefu.Za nini?Wakati huo huo uwe ushaagiza kwamba hakuna matangazo ya tv na redio zaidi ya yale ya washikaji wako wa karibu kwa ajili tu ya kutunza historia ili vijukuu vyako siku za mbeleni vijue babu alikuwa mtemi.Mchezo unakuwa umekamilika.

 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 8:58 PM | Permalink | Maoni 8
Wednesday, January 02, 2008
KHERI YA MWAKA MPYA.MAAZIMIO?

Kheri ya mwaka mpya msomaji wangu. Nimekuwa kimya kidogo,naelewa.Mambo yalikuwa mengi mwishoni mwishoni mwa mwaka.Familia,watoto,ndugu,jamaa,kazi,maisha ya ughaibuni nk.Msururu wote huo,kwa njia moja au nyingine,unahitaji atensheni yangu.Silalamiki lakini,nasema tu.Ndio hali halisi ya maisha.Ukishazaliwa mtoto wa kiume tena ndio inakuwa balaa.

Vipi wewe? Sherehe za xmas ulizisheherekea vipi?Mwaka mpya umeuanzaje?Hapa nilipo ni baridi mtindo mmoja.Wakati mwingine unatamani uishi ndani ya friji ili ujue moja.Huu ndio ule wakati wa korodani kunyweeea.Kama huna nguvu ya ziada,kazi kwako.Unaweza paniki ukakimbilia kale ka kidonge kanakoanzia na herufi V.Nyakati nyingine huwa najiuliza kama ulikuwa mpango wa Mungu watu waishi upande huu wa dunia.Nasema hivyo nikizingatia jinsi zama hizo zilivyokuwa.Hakuna nguo za sufi kama tulizonazo hii leo,hakuna magari yenye vileta joto kama hivi leo.Hakuna nyumba zilizo na majiko ya humo kwa humo.Sasa waliishije hao watu wa mwanzo huku?

Kwa upande mwingine,hainishangazi kusikia zile habari za kisayansi na historia kwamba fuvu la kale kabisa lilipatikana kule Tanzania.Naam..kule kunafaa kuishi,ndio mpango wa Mungu.Ajabu sisi wenyewe hatujui uzuri wa kwetu.Tukiona vinaelea tunadhani vimeshushwa..kumbe.Ndio maana profesa mmoja aliwahi kuuliza Waafrika Ndivyo Tulivyo? Wengine wakamjia juu...sijui walikuwa wanafikiria nini.Hata hivyo kwetu kunabakia kuzuri.Kwetu unaweza ukalala mzungu wa nne na wala usikauke kwa baridi kali.Tatizo mbu watakavyokutandika..utakoma.Hutorudia tena.

Sasa usije ukadhani sipendi kabisa kuishi huku.Ama!Ughaibuni kuna raha zake.Karaha nazo zipo lakini wenzetu wanajitahidi sana kila siku kuzidhibiti.Mpaka kahawa unaweza kununua ukiwa umekaa ndani ya gari yako tu.Kama sio uvivu ni nini hicho?Halafu wenyewe wanashangaa kwanini wananenepeana kama viboko.Kila unachokiona kwenye luninga ni kuhusiana na unene vs wembamba.Mwaka mpya unapoanza kama hivi,mamilioni ya watu(hususani wanawake) wanadhamiria kupunguza uzito wao.Yaani huku mwanamke asiye na nyama au minofu ndio anayevutia zaidi.Haingii akilini hii..au sio? Kama nakuona vile.Huku ughaibuni husikii kitu umeme umekatika wala maji.Ukifungua bomba...hayoo..meupee.Umeme ukikatika inakuwa ni breaking news.Utawasikia wazungu..can you believe this?Nami nawajibu..I know..I can’t believe this!Kichwani nawaambia..mngejua kwetu umeme unakatika kutwa mara sita na wakati mwingine unakaa hata wiki bila kurudi na bila kusikia neno lolote achilia mbali samahani kwa wahusika,mngebana ngenge.

Enewei,nakutakia kheri ya mwaka mpya.Tusukume sote gurudumu la maendeleo...hata kama limekwama kwenye lindi la tope zito.Kabla sijasahau,umesikia ahadi kutoka kwa wapinzani nchini Tanzania?Wamesema huu ni mwaka wa kupigania katiba mpya nchini Tanzania.Katiba iliyoandikwa na wananchi na sio hii yenye harufu mbaya ya kikoloni na sisi kwa ujuha wetu tunaishia kuweka viraka tu kila kukicha! Wapinzania wanataka pia tume huru ya uchaguzi.Hii ya sasa ndio kama hivyo ilivyo.Haina meno,jaji wa serikali ndio mwenyekiti wa tume.Kwani hujasikia yaliyotokea huko Kenya?Mwenyekiti wa Tume anasema eti alipomtangaza mshikaji wake Mwai Kibaki kuwa mshindi alikuwa “under pressure”.Msalie mtume,hivi lini tutastaarabika sisi?Wenzetu wakitushangaa eti tunakasirika,tunawaita wabaguzi na wachimba chumvi.Mitusi inayotutoka huku mishipa yote ya fahamu ikiwa imetutoka,sio ya kawaida.

Kheri ya mwaka mpya msomaji.Kama unapenda uandishi wa namna hii niambie niendelee.Nimechoka ule uandishi wa kiprofesa.Simple 2008.Ndio azimio langu.

 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 11:28 AM | Permalink | Maoni 9
Monday, December 17, 2007
PIGANIA UHURU WA KUJIELEZEA
Miaka michache iliyopita kulikuwa hakuna blogs. Kama ulitaka kusikika ilibidi utumie mlolongo mrefu sana. Mmojawapo ulikuwa ni ule wa kuandika barua kwa "mhariri".Na yeye,kutegemea na utashi wake au hongo aliyopokea juzi pale alipokutana na "mheshimiwa" katika ile baa karibu na wanaporandaranda "madada poa"(nasikia siku hizi wameingiliwa na makaka poa pia),mara nyingi zilikuwa zinaishia kapuni.

Matumizi ya blogs au uandishi huria kama ambavyo wengine wamependa kuuita, yameleta mapinduzi mapya. Bado yanaendelea kuleta mapinduzi mapya. Leo hii naweza kuandika na wewe ukasoma bila kupitia mlolongo mrefu. Unachotakiwa kuwa nacho ni tarakilishi na muda tu. Kizuri zaidi ni kwamba unaposoma nilichoandika unaweza kuchagua kukubaliana nami,kupingana nami au kunibeza tu na kuondoka zako kwenda uendako. Katika makundi yote hayo matatu unao pia uwezo wa kuniachia "vidonge" vyangu. Unaweza ukasema kwanini unakubaliana nami au unapingana nami. Mambo yanakwenda hivyo. Bila kurushiana ngumi wala kukunjiana ndita,tunaelimishana,tunajenga jamii.

Nasi, bila kukaa ndani ya yale masinagogi ya waandishi, tunaandika. Ukiamua kutuita waandishi au wacheza mduara ni juu yako.Tunachojua ni kwamba hivi sasa tuna uwezo wa kuandika na tukasomwa kuliko yule bwana mhariri mkuu.

Tatizo linakuja kwamba watawala walio wengi, wale ambao maisha yao yamejaa longolongo kila kukicha,huwa hawataki kusikia kitu kinachoitwa "uhuru wa kujielezea' achilia mbali uhuru wa vyombo vya habari wala waandishi. Ndio maana kuna mashirika au oganaizesheni kama PEN ambazo kazi yake kubwa ni kutetea uhuru wako wa kuandika,kusomwa nk. Hebu watembelee hapa, usichelee kujiunga nao. Soma visa mbalimbali vinavyowakuta waandishi. Pigania haki yako ya kujielezea.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 6:29 PM | Permalink | Maoni 1
Sunday, November 18, 2007
HAPPY TANZANIA BLOG DAY?

Mwaka mmoja uliopita wanablogu wa kitanzania tuliweka historia mpya.Siku kama ya leo,yaani tarehe 18 Novemba 2006 kuanzia saa sita mchana kwa saa za Tanzania,wanablogu wa kitanzania tuliotapakaa dunia nzima tulikutana kwa minajili ya kuunda jumuiya yetu rasmi na kuwa na siku ya blogu Tanzania.Katika mkutano ule tuliipitisha rasmi siku ya tarehe 18 Novemba kila mwaka kuwa siku ya blog Tanzania.Kwa maneno mengine,leo ni Tanzania Blog Day.

Naikumbuka vyema siku ile kwani sio tu nilidamka asubuhi na mapema(ili niwahe mkutano uliokuwa umetegwa kwa masaa ya Tanzania ingali nipo Canada) bali pia sote tuliohudhuria mkutano ule tulikuwa tuna shauku ya kuunda jumuia ambayo italeta mabadiliko ya kijamii hususani kuhusu jinsi tunavyopashana habari na pia kuchangia katika uundwaji au ubomoaji wa sera za nchi.Huo ndio muelekeo wetu ambao nina uhakika bado tunalo jukumu la kuuendeleza kwa hali na mali.Siku ile sote tulikuwa na mioyo ya kimapinduzi na upendo wa aina yake kwa taifa letu,jamii zetu na dunia yetu kwa ujumla.

Usingeweza kututofautisha na kina Fidel Castro,Che na wenzao walipokuwa wakipanga mikakati ya kimapinduzi enzi zile.Tofauti kati yetu na wao ni kwamba wao walikuwa na silaha za wazi wazi kama bunduki na mijeledi.Sisi tulichokuwa nacho na ambacho naamini bado tunacho ni uhuru wa kupashana habari na kuwasiliana kwa minajili ya kuleta mabadiliko ya kijamii.Hii ndio jamaa wa Global Voices wanaiita Blogging For Social Change!Ingekuwa zamani tungesema tulikuwa tunachukua ule msimamo kwamba A Pen is Mightier Than A Sword.Tatizo ni kwamba zama hizi zinatumia zaidi “keyboard”kuliko kalamu ya kawaida au Bic kama wengi wetu tulivyozoea enzi zile.Kwani mmesahau kwamba kuna wakati tulikuwa tunahitimu kutumia penseli na kisha tunahamia kwenye kutumia bic?Hivi ilikuwa darasa la ngapi vile?

Tungekuwa tunaenda kwa ule mwendo wa kichama chama, leo ingekuwa ndio siku ya gwaride,mapambio,mashati au t-shirts za rangi za vyama,hotuba,vipeperushi, ahadi na mambo kama hayo. Tungekutana pale bwalo la maofisa na kutumia fataki za ule mvinyo wa kizungu(champagne) utadhani tumeshafanikiwa kuitokomeza vita ya njaa,maradhi na umasikini.Ungetuona usingedhani kama tunaishi kwenye nchi yenye raia kibao wanaolala njaa,wanaolala nje,mitaani,chini ya magari,yenye raia wengi wanaopoteza maisha kutokana na ukosefu wa huduma za afya na kero zingine chungu mbovu.Hapo sijataja wanaopasua kichwa badala ya mguu.Hebu tuachane na hayo,ngoja niendelee na ajenda ya leo ili nisije nikakukwaza ndugu msomaji bure.

Baada ya mkutano ule wa kihistoria tulichagua viongozi.Palikuwa na kampeni,japo za chini chini,tukapata fursa ya kukagua wasifu wa baadhi ya wagombea nk.Demokrasia ikachukua mkondo wake,tukapata viongozi.Hapakuwa na shampeni wala ulanzi lakini sote tulifurahi na bado tunafurahi kwamba tunao viongozi.Lakini nisingependa tusahau kwamba hata kabla ya kukutana rasmi na baadaye kupata viongozi,kuna wakati tulishapata “Azimio la Dodoma”.Si unakumbuka tulivyowekeana maadili ya maana?Tatizo wale jamaa waliokutana Dodoma na baadaye sisi kuamua kulikubali azimio lao,wote wamepotea kwenye ulimwengu wa blog hivi leo.Blog zao zimeanza kuwa kama zile ofisi za masijara za ile wizara pale karibu na wanaposhinda kutwa nzima vijana wanaoojiita “misheni tauni”.Najiuliza hapa,hivi nikiwatajia yale majina ya wana-Dodoma mtanisaidia kuwauliza nini kimewasibu?Au na wao kuna mlungula umetembea ili kuwazima?Sijui.

Pamoja na kupata viongozi na matumaini mapya,leo naomba nisiwe mnafiki bali niseme wazi kwamba,kuanzia pale mambo kwa kiasi fulani yakaanza kwenda taratibu mno.Sababu zaweza kuwa nyingi na tofauti.Lakini ukweli utabakia(kwa mtizamo wangu) kwamba kuna kasi imepotea ambayo hatuna budi kuirudisha kwa kasi pia.Mfano mzuri ni jinsi ambavyo siku hii ya leo tunaikumbuka.Si unakumbuka kwenye mkutano kuna jamaa aliniahidi kwamba leo atanipa mvinyo tani yangu?Au wewe umesahau?

Yote tisa,kumi ni swali ambalo leo limegubika moyo wangu.Swali hilo ni je wangapi kati ya wanablogu waliohudhuria mkutano ule na hata wale ambao hawakuhudhuria lakini baadaye wakatambua yaliyojiri mkutanoni siku ile wanaikumbuka siku hii muhimu?Na je mbona viongozi wetu hata hawakuchukua jukumu la kuikumbusha jamii kuhusiana na siku hii?Nini kimetokea?Kama na wewe msomaji wangu umesema,ah hivi kweli eenh,todei wi wea sapozidi tu rimemba endi selebreiti bulogu dei,basi jua tuna tatizo.Mimi na wewe.Wala usipande darini ukadhani utakuwa salama.Kunguni wako kila sehemu,shauri yako.

Kwa mfuatiliaji wa maendeleo ya blogu za kitanzania,atakubaliana na mimi kwenye jambo moja muhimu.Msisimko uliokuwepo hapo mwanzo mwanzo,haupo tena.Unazikumbuka enzi zile za kumkaribisha kila mwanablogu mpya kwa maneno matamu na ya kutiana moyo?Kila mtu mpya “alipokata shauri” na kuamua kufungua blogu sote tulifahamishana.Tukachukua dakika chache za kukaribishana na kutakiana heri.Tulikuwa na ujamaa wa aina fulani ambao binafsi niliupenda sana.Mpaka leo hii napata faraja nikitembelea “post” yangu ya kwanza kabisa na kuona jinsi wanablogu walioanza kabla yangu walivyonikaribisha na kunitakia kheri.Whati hapenedi?

Ni wazi kwamba tunafanya makosa.Tunafanya makosa ya kuzipuuza zama hizi mpya za mawasiliano ya umma(mtazamo wangu).Kwanza sitaki kuamini kwamba tunazipuuza au tumeanza kuzipuuza. Sitaki kabisa kuwaza namna hiyo kwani nikifanya hivyo siku si siku itabidi mnipeleke Dodoma.Wenzetu,kwa mfano wakenya na waganda wanaendelea kuzikumbatia zama hizi kwa marefu na mapana.Sisi bado tunaenda kwa mwendo wa kinyonga.Tuna haja ya kuanza tena kukimbia.Tuna kila sababu ya kuzidi kuungana,kuzidi kuwaalika watanzania wengine wenye maarifa tofauti tofauti kufungua blogs zao,tena za Kiswahili ili sio tu tukuze lugha yetu bali tuongee tuelewane.Tusipofanya hivyo tunazidi kuwaachia wenzetu fulani fulani,wa ndani na nje ya nchi,waamue mustakabali wa maisha yetu.Nasema hivi kwa sababu moja,usiposema kupitia kwenye mawasiliano ya umma kama blogs,utasema kupitia wapi?Kwenye pishi la pilau na kanga kutoka barahindi?

Ubaya au uzuri wa zama mpya mara nyingi huwa zinahitaji kuoteshwa ili baadaye ziweze kuota mizizi na kutupa matokeo tunayoyahitaji.Raisi Museveni wa Uganda ana kitabu chake kizuri sana kinachoitwa Sowing The Mustard Seed(ukikipata kisome).Jukumu hilo la kuotesha ni letu sote.Viongozi kazi yao ni kutuongoza tu,watendaji ni sisi sote.Tusikubali kutupa mti na jongoo wake. Kama umekaa pembeni ukisubiri wenzio wakuoteshee mbegu kwanza unafanya lisilo jema.Fikiria upya.

Mwisho naomba niwatakieni wote Happy Tanzania Blog Day.Najua hata kama hakuna shangwe na vigelegele mwaka huu,basi mwakani huenda tukawa nao.Tutazichagua blog bora na kuwapa waongozaji wake japo bilauri ya mpingo ili wakanywee ndani yake wakikumbuka kesho yake wanatakiwa kuendeleza libeneke kama rafiki yangu Issa Michuzi anavyopenda kusema.Tuko pamoja ndugu zangu katika blogu.Nalia lakini..usinione hivi.

 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 1:06 AM | Permalink | Maoni 5
Tuesday, November 06, 2007
UNATAKA KUUA SIMBA? KARIBU TANZANIA

Utalii ni mojawapo ya vyanzo muhimu sana vya mapato vya serikali yetu ya Tanzania.Mbuga zetu za wanyama ni fahari yetu na majaaliwa aliyotupa mwenyezi mungu. Lakini ili tuendelee kuwa na wanyama hao ambao ndio chambo cha biashara ya utalii,hatuna budi kuwatunza kama sio kuwalinda. Wenzetu

Kenya wao hawaruhusu uwindaji wa wanyama.Kwetu sisi rukhsa,hela yako tu.Tunakupa bunduki,wachuna ngozi na watu wa kukuongoza msituni ukamuue simba,swala,pundamilia na takribani mnyama yeyote unayetaka! Hata kama unaweza kumuua kama vile "morani" wa kimasai poa tu. Soma habari kamili kwa kubonyeza hapa.

 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 10:24 AM | Permalink | Maoni 9
Saturday, October 20, 2007
LAZIMA TUWE NA DEMOKRASIA?
Swali lililopo kwenye kichwa cha habari hapo juu linaweza kuwa rahisi sana usipofikiria kwa makini. Jibu la haraka haraka ni ndio, demokrasia ni lazima,ndio ubinadamu na utu kama sio kwenda na wakati.

Pamoja na hayo demokrasia bado ni mjadala mpana sana kwa sababu kila mtu anaweza akawa na maana yake na sote tukadai kuwa sawa na mwalimu akatuwekea ile alama ya vyema huku ikiwa na kimkato kidogo. Lakini je demokrasia ni suala la lazima?Sisi kama wananchi,walimwengu,binadamu wa karne hii ya 21 tunahitaji demokrasia? Na je, ungepewa nafasi ya kumchagua raisi wa dunia ungemchagua nani? Ni kweli kwamba wanawake ni mabingwa wa demokrasia kuliko wanaume? Ili kujibu maswali hayo na mengineyo mengi kuhusiana na suala zima la demokrasia,vijana fulani kutoka Afrika Kusini wameanzisha mjadala mkubwa kabisa mtandaoni kuwahi kutokea kuhusu suala hili. Tembelea tovuti ya Why Democracy?ujiunge katika mjadala, tizama documentaries, na kupanua mtazamo wako kuhusu demokrasia. Bonyeza hapa.
 
Muandishi: Jeff Msangi |Tarehe: 3:02 PM | Permalink | Maoni 4
   
 
Copyright 2006 © JEFF MSANGI. All Rights Reserved
 
Idadi ya watu Idadi ya watu Idadi ya watu
eXTReMe Tracker